Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mvua zaleta matumaini kwa wakulima wa Syria:FAO/WFP

Mvua zaleta matumaini kwa wakulima wa Syria:FAO/WFP

Uhakika wa chakula katika baadhi ya sehemu nchini Syria umeimarika kiasi ulilinganisha na wakati kama huu mwaka jana kutokana na kuimarika kwa usalama , mvua na kuwezesha kupatikana kwa fursa ya kufikisha misaada ya kibinadamu , lakini hali ya ujumla nchini humo bado ni mbaya zaidi kuliko kabla ya vita , yameonya leo mashirika mawili ya Umoja wa Mataifa.

Tathimini mpya ya mazao na uhakika wa chakula iliyofanywa na shirika la chakula na kilimo FAO na shirika la mpango wa chakula duniani WFP inakadiria kwamba uzalishashi wa ngano hivi sasa ni tani milioni 1.8, ambayo ni asilimia 12 zaidi ya mwaka jana , japo bado ni chini ya nusu ya ilivyokuwa kabla ya vita.

Tathimini hiyo iliyotolewa leo pia inakadiria kwamba Wasyria milioni 6.9 bado hawana uhakika wa chakula huku wengine milioni 5.6 huenda wakaukosa uhakika huo bila msaada wa mgao wa chakula wanaopokea kila mwezi.

Hata hivyo FAO na WFP wanasema kwa baadhi ya familia kuna nuru gizani kwani licha ya changamoto kilimo kinaendelea kuzalisha chakula kwa ajili ya Syria na wakulima wengi zaidi wanatarajiwa kupata fursa ya kulima tena mashamba yao hasa ukizingatia mvua zinazonyesha zimeleta matumaini.