Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Gharama za vita kwa binadamu Afghanistan ni kubwa mno:UM

Gharama za vita kwa binadamu Afghanistan ni kubwa mno:UM

Gharama za vita vya Afghanistan kwa binadamu ni kubwa mno amesema mkuu wa mpango wa Umoja wa Mataifa nchini humo , akitaja vifo, uharibifu na madhila kwa raia.

Tadamichi Yamamoto ametoa kauli hiyo kufuatia ripoti ya mpango wa Umoja wa Mataifa UNAMA na ofisi ya kamishina mkuu wa haki za binadamu iliyotolewa leo.

Ripoti imebaini kwamba jumla ya raia 1,662 walikufa kati ya Januari Mosi na Juni 30 mwaka huu ikiwa ni ongezeko la asilimia 2 ukilinganisha na wakati kama huu mwaka jana.

Asilimia 40 ya raia walioathirika katika kipindi hiki cha miezi sita , waliuawa au kujeruhiwa na vikosi vinavyopinga serikali kwa kutumia vifaa vya mlipuko kama vile mabomu ya kujitoa muhanga au magruneti.

Takwimu za ripoti hiyo pia zinaonyesha ongezeko la idadi ya wanawake na watoto waliouawa na kujeruhiwa , na kugeuza ukurasa wa mwaka 2016 ambapo idadi ilionekana kushuka.

Ripoti hiyo imetoa mapendekezo kadhaa yakiwemo wito kwa majeshi yanayopinga serikali kuacha kuwalenga raia na kutekeleza amri ya uongozi wa kundi lenye itikadi kali la Taliban, na pia kukomesha mashambulizi ya aina hiyo