Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Utekelezaji wa mkataba wa Disemba 2016 DRC hauridhishi-UM

Utekelezaji wa mkataba wa Disemba 2016 DRC hauridhishi-UM

Utekelezaji wa mkataba uliotiwa saini mwaka 2016 mwezi Desemba nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, hauridhishi huku hali ikiendelea kuwa tete katika maeneo mbalimbali hususani ya Mashariki na Magharibi mwa nchi hiyo.

Hayo yamesemwa na Jean-Pierre Lacroix mkuu wa idara ya operesheni za ulinzi wa amani ya Umoja wa Mataifa, akiwasilisha ripoti leo jumanne mbele ya baraza la usalama la Umoja wa Mataifa. Amesema mosi utekelezaji wa makubaliano hauridhishi pili..

(SAUTI YA LACROIX)

“Hali ya usalama katika baadhi ya maeneo ya mashariki na magharibi mwa nchi hiyo imeghubikwa na ongezeko la machafuko na mapigano baina ya vikosi vya serikali na makundi yenye silaha , hali ambayo imechangia hali mbaya ya ongezeko la ukiukwaji wa haki za binadamu , hali hiyo ya usalama pia ni chanzo cha kuzorota kwa hali ya kibinadamu . Na kwa mukhtada huo hii itakuwa point yangu ya tatu MONUSCO inafanya kila njia kukabiliana na changamoto zinazoikabili DRC.”

Katika mkutano huo ambao ulijikita katika hali ya kisiasa, kiusalama na kibinadamu nchini DRC, Lacroix amesema suala lingine linalotia hofu ni ongezeko la hivi karibuni la machafuko ya kikabila kwenye jimbo la Kasai, akitolea mfano ghasia kati ya jamii za Pende na Tshokwe zinazounga mkono serikali na jamii za Luba na Lulua zinazounga mkono wanamgambo wa Kamuina Nsapu yaliyosababisha vifo vya watu 38 mwezi Aprili.

Ameongeza kuwa licha ya juhudi zinazofanyika kurejesha utulivu hali bado ni tete na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu unaripotiwa kila uchao. ikiwemo kupatikana kwa makaburi ya pamoja zaidi ya 40.

Hata hivyo amesema licha ya changamoto zote hizo katika upande wa kisiasa kuna matumaini hasa kwenye uandikishaji wapiga kura kwa ajili ya uchaguzi unaotarajiwa baadaye mwaka huu..

(LACROIX CUT 3)

“Hatua zilizopo katika uandikishaji wa daftari la wapiga kura katika majimbo 24 kati ya 26 ya DRC ni ishara inayotia moyo chini ya usimamizi wa tume ya uchaguzi na kwa msaada wa MONUSCO hadi Julai 10 takribani wapiga kura milioni 33 wameshaandikishwa kati ya wapiga kura milioni 44 wanaokadiriwa.”

Amesema pamoja na mafanikio hayo bado kuna changamoto ya ucheleweshwaji wa kutoa tarehe ya uchaguzi na fedha za kufadhili uchaguzi huo.