Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maendeleo endelevu bila kujali haki za binadamu ni bure- Mtaalamu

Maendeleo endelevu bila kujali haki za binadamu ni bure- Mtaalamu

Wakati dunia inaendelea na mchakato wa kutekeleza malengo ya maendeleo endelevu, SDGs, serikali na wafanyabiashara wametakiwa kuweka sheria na kanuni zinazoweka mbele maslahi ya watu na si faida.

Wataalamu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa wamesema hay oleo huko Paris, Ufaransa wakati wa mkutano wa kimataifa kuhusu maadili ya kibiashara ya uwajibikaji.

Mmoja wao Anita Ramasastry amesema maendeleo yasiyojali haki za binadamu ni bure kabisa na yanapoteza maana ya maendeleo endelevu.

Mathalani amesema miradi ya nishati endelevu inayosababisha watu wa jamii ya asili kufurumushwa maeneo yao bila ridhaa au kushirikishwa haitakuwa na maana.

Bi. Ramasastry amesema njia thabiti ya sekta ya biashara kuchagiza maendeleo ni kujumuisha haki za binadamu katika kila operesheni na mifumo yao ya utendaji hata ile ya ajira.