Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sharti la kufunga Al Jazeera ni pigo kwa uhuru wa habari- Mtaalamu

Sharti la kufunga Al Jazeera ni pigo kwa uhuru wa habari- Mtaalamu

Kitendo cha nchi Nne za kiarabu kutaka Qatar ifunge chombo chake cha habari Al Jazeera kama moja ya masharti 13 ya kuondolewa vikwazo dhidi yake ni za kusikitisha.

Mtaalamu maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu uhuru wa kujieleza David Kaye amesema hayo leo akigusia sharti lililotolewa na Saudi Arabia, Bahrain, Misri na Falme za kiarabu ambazo zimekata uhusiano wa kidiplomasia na kiuchumi na Qatar.

Bwana Kaye amesema kufunga Al Jazeera ni pigo kubwa kwa eneo hilo ambalo tayari limegubikwa na vikwazo lukuki vya kuripoti habari.

(Sauti ya Kaye)

“Hii bila shaka ni hatua ya kionevu. Unafahamu kukabiliwa kwa mfano na sharti la kuchuja habari mtandaoni, kufunga baadhi ya wavuti pengine siyo zote za habari. Serikali zinapaswa kuona aina hii ya sharti kuwa ni tishio kwa nchi zote na kwa uhuru wa kupata taarifa.”

Ametoa wito kwa jamii ya kimataifa kusihi nchi hizo nne zisitekeleze sharti lao dhidi ya Qatar na kujizuia kudhibiti vyombo vya habari kwenye nchi zao.