Mkutano wa bahari umefanikiwa, lakini kazi itaendelea:UM
Siku tano zilizoghubikwa na mikutano, mijadala na vikao takribani 150 na maonyesho 41 katika mkutano wa kimataifa wa bahari kwenye makao makuu ya umoja wa Mataifa hapa New York hatimaye zimefunga mlango hii leo ijumaa.
Mkutano huo wa bahari uliowaleta pamoja wadau mbalimbali zaidi ya 1000, zikiwemo nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa, watalaamu wa sanyasi, mashirika ya kimataifa na asasi za kiraia, na ulijikita katika mada mbalimbali zinazohusu lengo nambari 14 la maendeleo endelevu , maisha chini ya maji.
Kikubwa kimekuwa ni kuangalia uhifadhi, matumizi endelevu ya bahari na rasilimali zake, changamoto na suluhu.
(SAUTI YA ISABELLA)
“Hali ya bahari ni mbaya, ya kusikitisha na pia kutia hofu, na inatuathiri sote na mkutano huu wa bahari umekuwa ni fursa yetu ya kubadili ukurasa, huu ni mwanzo na hakuna kurudi nyuma na naamini utashi wa kisiasa uliodhihirika wiki hii, pengine ndio matokeo muhimu zaidi wiki hii, na sasa kibarua kigumu kinaendelea.”
(SAUTI YA WU)
“Tuko tayari kusaidia nchi wanachama na wadau wengine katika mchakato unaofuata kwa kupitia uchambuzi na uwezeshaji , kubadilisha uzoefu na yale tuliyojifunza”
(SAUTI YA THOMSON)
"Nimeridhika kwa asilimia 100, tulichokitaka kwenye mkutano huu tumekipata, na kitu kimoja nilicho na uhakika nacho kutoka kwenye mkutano huu na kuendelea hakuna mtu atakayesema hatukufahamu hali ilikuwa mbaya kiasi gani, hatukujua kwamba kutakuwa na maplastiki mengi baharini kuliko samaki ifikapo 2050, kiwango cha uelewa wa matatizo baharini kimepandishwa."