Watu laki 700,000 Nigeria wanahitaji msaada haraka:UM

Watu laki 700,000 Nigeria wanahitaji msaada haraka:UM

Takribani watu laki 7 ambao hawajafikiwa na misaada ya kibinadamu wanaishi katika hali ya taharuki Kaskazini Mashariki mwa Nigeria na wanahitaji msaada wa haraka umesema Umoja wa Mataifa Jumanne.

Uasi wa Boko Haram ambao sasa inaingia mwaka wa nane umekatili maisha ya watu zaidi ya 20,000 na kusababisha wengine milioni 1.8 kuzikimbia nyumba zao.

Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu misaada ya kibinadamu OCHA, wakimbizi wengi wanarejea nyumbani kutoka Cameroon na nchi nyingine jirani katika wiki za karibuni kwa sababu ya mgogoro wa muda mrefu wanakosa huduma za msingi.

Akizungumza mjini Geneva Edward Kallon mratibu wa masuala ya kibinadamu Nigeria, ameonya kuhusu hali mbaya ya kibinadamu hususan kwa wanawake na watoto akisema watu milioni 6.9 wanahitaji msaada wa haraka kuokoa maisha yao hasa wakati huu kukiwa na tisho kubwa la baa la njaa.

Amesema watu 7500 wakiwemo wanaume, wavulana na wanawake wameripoti kufanyiwa ukatili wa kingono tangu kuanza kwa machafuko miaka minane iliyopita.

Pia shirika hilo limeonya kuwa watoto 450,000 wako hatarini kufa kutokana na maradhi yanayohusiana na utapia mlo.