Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

IAEA yapata mshirika wa kuboresha tiba ya maradhi ya moyo

IAEA yapata mshirika wa kuboresha tiba ya maradhi ya moyo

Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomiki (IAEA), leo limekubaliana na shirika la Kimarekani la matibabu ya moyo kutumia teknolojia ya nyuklia (ASNC) kuwa na ushirikiano katika kuboresha huduma za afya kwa watu wenye maradhi ya moyo kote duniani.

Ushirikiano huo utajumuisha kuimarisha mafunzo ya wataalam wa afya katika nchi za kipato cha chini na cha wastani, ili waweze kupima na kutathmini kiwango cha maradhi ya moyo miongoni mwa wagonjwa.

Maradhi ya moyo huua watu wengi zaidi kuliko sababu nyingine yoyote ile ya kifo, yakikatili uhai wa zaidi ya watu milioni 17.5 kila mwaka, sawa na asilimia 31 ya vifo vyote duniani.

Kupitia ushirikiano huo, IAEA na ASNC zitaendeleza vifaa vya mafunzo kwa ajili ya kitengo cha IAEA cha afya ya binadamu, ambacho ni wavuti unaotembelewa na zaidi ya wataalam 5,000 wa afya. Aidha, ASNC itawaweka wataalam wake tayari kwa ajili ya ziara za kutoa ushauri, pamoja na mafunzo, ikiwa ni sehemu ya ushirikiano wa kitaaluma.