Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Bilioni 1.1 zapatikana kusaidia Yemen, Guterres ataka ziwafikie walengwa.

Bilioni 1.1 zapatikana kusaidia Yemen, Guterres ataka ziwafikie walengwa.

Mkutano wa ufadhili kuhusu Yemen umekamilika mjini Geneva Uswisi, kwa kile kilichoelezwa kuwa ni mafanikio baada ya washiriki kuchangia kiasi cha dola bilioni 1.1

Lengo la awali ilikuwa kuchangia dola biloni 2.1 ili kuinusuru Yemen inayokabiliana na baa kubwa zaidi la njaa duniani, kutokana na mapigano ya wenyewe kwa wenyewe yanayoendelea nchini humo.

Akizungumza wakati wa kufungwa kwa mkutano huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amesema ameshawishika kwamba miezi ijayo kiwango cha fedha kilichosalia kitapatikana ili kuetekeleza mpango uliowekwa.

Amesema baadaya kupatikana kwa kiasi hicho cha fedha, kinachohitajika kwa sasa ni kuhakikisha pande kinzani zinaruhusu ufikishwaji wa misaada kwa walengwa kwa kuzingatia sheria za kimataiafa za kibinadamu, vinginevyo ahadi hizo za fedha hazina maana kama hazitowafikia raia.

Ameongeza kuwa Yemen inastahili msaada kwani imekuwa mstari wa mbele katika kuwapatia hifdhi raia wa mataifa mengine ambao wamefika nchini humo wakikimbia machafuko nchini mwao.