Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nchi nyingi duniani hazina maji safi ya kunywa: Ripoti

Nchi nyingi duniani hazina maji safi ya kunywa: Ripoti

Ripoti mpya iliyochapishwa na Shirika la Afya Ulimwenguni, WHO, kwa niaba ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Maji inaonya kuwa nchi nyingi hazijaongeza kasi ya kutosha kwa kutenga fedha ambazo zitatumika ili kufikia malengo ya maendeleo endelevu, SDGs kwa matumizi ya maji safi.

Ripoti hiyo inasisitiza kwamba nchi zinapswa kuongeza jitihada za kutambua vyanzo vipya vya fedha ili kuhakikisha upatikanaji wa maji safi ya kunywa na kudhibiti magonjwa ambayo yanasababishwa na watu kunywa maji machafu.

Akizungumza kuhusu ripoti hiyo, Dk Maria Neira, ambaye ni Mkurugenzi wa WHO kwenye Idara ya Afya ya Umma, Mazingira na masuala ya kijamii amesema karibu watu bilioni mbili wako hatarini kuambukizwa kipindupindu, kuhara damu, kupata homa ya matumbo na polio kutokana na kunywa maji machafu ambayo yanaweza kuwa na mchanganyiko wa kinyesi

Ameongeza kuwa maji machafu ya kunywa yanakadiriwa kusababisha vifo vya zaidi ya watu laki 500 000 kila mwaka.

WHO inasema kuwa nchi nyingi zinazoendelea, zina malengo ya kuhakikisha upatikanaji wa miundombinu ya msingi, ambayo itatoa huduma salama ya maji na ya kuaminika ili kufikia malengo ya maendeleo endelevu ifikapo mwaka 2030.

Katika ripoti hio, Benki ya Dunia inakadiria kwamba uwekezaji katika miundombinu wapaswa kuongezwa na hivyo kutahitajika dola za marekani bilioni 114 kwa mwaka.