Skip to main content

Mabaki ya miili ya wataalamu DRC yapatikana, UM kuchunguza

Mabaki ya miili ya wataalamu DRC yapatikana, UM kuchunguza

Hatimaye Umoja wa Mataifa umethibitisha kuwa mabaki ya miili yaliyopatikana huko Kananga, jimbo la Kasai Kati nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC ni ya wataalamu wawili wa kimataifa waliotoweka wiki mbili zilizopita.

Katika taarifa yake, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amesema walinda amani wa umoja huo walibaini mabaki hayo siku ya Jumatatu na kuthibitishwa kuwa ni ya Michael Sharp kutoka Marekani na zaidi Catalan kutoka Sweden.

Wawili hao walikuwepo DRC kuchunguza chanzo cha ukosefu wa usalama na mzozo na ili kusaidia kuleta amani nchini humo ambapo wakati wa kutoweka kwao walikuwa wameambatana na raia wengine wanne wa nchi hiyo.

Bwana Guterres ametuma salamu za rambirambi kwa wafiwa huku akisema kuwa wataenzi kazi za wataalamu hao wawili kwa kuendeleza jukumu lao la kundi la wataalamu.

Amesema anaamini kuwa serikali ya DRC itachunguza kisa hicho huku akisema kuwa Umoja wa Mataifa nao utachunguza na iwapo kuna uhalifu wowote watahakikisha haki inatendeka.

Katibu Mkuu ameisihi DRC iendelee kusaka raia wengine wanne akisema kuwa Umoja wa Mataifa utasaidia katika hatua hiyo.