Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR yatoa wito IGAD wa msaada Zaidi kwa Somalia:

UNHCR yatoa wito IGAD wa msaada Zaidi kwa Somalia:

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR,limetoa wito wa msaada kwa juhudi zenye lengo la kuleta utulivu ndani ya Somalia na kwa nchi zinazohifadhi wakimbizi wa Somalia.

Akizungumza kwenye mkutano maalumu wa wakuu wa nchi za shirika la kikanda la mendeleo IGAD unaofanyika Nairobi Kenya, kwa lengo la kusaka suluhu ya kudumu kwa mgogoro wa wakimbizi wa Somalia, kamishina mkuu msaidizi wa operesheni za UNHCR, George Okoth-Obbo, amezipongeza nchi jirani wa Somalia kwa wema wao wa kutoa ulinzi wa kimataifa kwa wakimbizi licha ya kuwa na changamozo zao binafsi za kiuchumi na kijamii , usalama wa taifa na mazingira.

UNHCR imetoa wito wa wajibu wa kimataifa kushirikiana na kanda ambako jamii zimekuwa zikihifadhi na kushirikiana rasilimali chache zilizopo na wakimbizi wa Somalia kwa miaka mingi.

image
Wakimbizi wa Somalia wakiwa Ethiopia moja ya nchi wanachama wa IGAD wakisubiri msaada. Picha kwa hisani ya UNHCR.
Pia shirika hilo limesisitiza wito wa haja ya kulinda fursa ya hifadhi kwa wakimbizi wa Somalia ambao hawawezi kurejea nyumbani na limezichagiza nchi kukumbatia ujumuishwaji katika jamii hasa kwa wakimbizi mbao mfano wameoa au kuolewa na raia.

Mkutano huo wa IGAD pampja na mambo mengine umezungumzia suala la kurejea nyumbani kwa hiyari kuwa sio chaguo pekee kwa wakimbizi na kutaka mshikamano wa kimataifa na wajibu wa kushirikiana kupitia kuwapa makazi ya kudumu wakimbizi wa Somalia na kuruhusu njia za kwenda kuishi taifa la tatu kama vile kusafirishwa kwa matibabu, usajili wa mipango ya kibinadamu, kukutanishwa na familia zao, na fursa za kazi kwa wahamiaji wenye ujuzi, pia kuhama kikazi na kupata elimu.

Zaidi ya Wasomali milioni mbili wametawanywa katika moja na migogoro ya muda mrefu sana duniani . Pia inakadiriwa kuna wakimbizi wa ndani milioni moja Somalia na wakimbizi wengine 900,000, wengi sasa wakiwa ni kizazi cha tatu. Wengi wao wako nchini Kenya, Ethiopia, Yemen, Uganda na Djibouti.