Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto Syria taabani-UNICEF

Watoto Syria taabani-UNICEF

Mkurugenzi wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF kanda ya Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini Geert Cappelaere amesema ripoti ya kwamba makumi ya watoto ni miongoni mwa watu 53 waliouawa jana jumatano kufuatia shambulio kwenye shule moja huko Syria, zinakumbusha ulimwengu kuwa jamii ya kimataifa inawaangusha watoto wa nchi hiyo.

Akizungumza wakati pande kinzani zinaanza kukutana Geneva, Uswisi kesho Ijumaa kwa mazungumzo, Cappelaere amesema watoto na vijana wanaporwa mustakhbali wao kutokana na jamii ya kimataifa kushindwa kuafikiana juu ya vita vya Syria ambavyo sasa vimeingia mwaka was aba.

Amesema vijana na watoto hao wanashindwa kwenda shule kupata elimu ambayo ni haki yao ya msingi huku familia zikikimbia makazi yao ili kusaka usalama.

Watoto hao waliouawa jana walikuwa wamesaka hifadhi kwenye shule moja huko Ar-Raqqa, kaskazini mashariki mwa Syria baada ya kukimbia makazi yao.

Bwana Cappelaere ametaka pande kinzani kwenye mzozo wa Syria na wengine wenye ushawishi na Syria kuongeza juhudi ili suluhu ya kisiasa ipatikane.