Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

FAO yaleta unafuu kwa wanawake wanaofuga kuku Gambia

FAO yaleta unafuu kwa wanawake wanaofuga kuku Gambia

Shirika la chakula na kilimo duniani, FAO limesema miradi yake katika nchi za Afrika imeanza kukwamua wanawake wajasiriamali kwa kuwawezesha kuinua vipato na wakati huo huo kuhakikisha upatikanaji wa chakula.

Afisa mwandamizi FAO anayehusika na usawa wa kijinsia na maendeleo vijijini Thacko Ndiaye amesema hayo katika mahojiano na Idhaa ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani ambako anahudhuria mkutano wa 61 wa kamisheni ya hali ya wanawake duniani, CSW61.

Ametolea mfano mradi wa ufugaji wa kuku nchini Gambia ambako amesema awali wanawake licha ya kuwa na ari ya kuleta maendeleo, walishindwa kuhimili kutokana na chakula cha kuku kuwa bei ghali kwa sababu kinaagizwa kutoka nje ya nchi, lakini hivi sasa..

(Sauti ya Thacko)

“Kwa hiyo kupitia mfuko wa mshikamano wa Afrika, FAO hivi sasa kwa kushirikiana na serikali ya Gambia inatekeleza mradi wa kuwezesha wanawake watengeneze chakula cha kuku ili wasiagize tena kutoka nje ya nchi.”

Halikadhalika ametaja mradi wa FAO wa teknolojia ya kukausha samaki, FST unaotekelezwa katika nchi 10 barani Afrika akisema teknolojia hiyo.

(Sauti ya Tacko)

“Inatoa hakikisho la upatikanaji wa chakula, wanawake hawako tena hatarini kuvuta moshi ndani ya nyumba, ambao ni hatari kwa afya yao. Wanaweza pia kukausha samaki wengi kwa wakati mmoja hi vyo inaokoa muda, wanaweza pia kuuza bidhaa hiyo kwa ubora zaidi.”