Skip to main content

Kama serikali haiwezi kutoa huduma ya maji basi isiwe jinai kuyatafuta:UM

Kama serikali haiwezi kutoa huduma ya maji basi isiwe jinai kuyatafuta:UM

Mtaalamu wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki ya binadamu ya maji na usafi ameelezea hofu yake kuhusu mswada wa sheria wa hivi karibuni mjini Lagos Nigeria unaoharamisha utafutaji wa maji kupitia mali asili.

Mwakilishi huyo maalumu Léo Heller, amesema wakati ambapo serikali inashindwa kutoa fursa ya kupata maji ya kunywa kwa watu wake , basi isiharamishe au kutoza faini kwa watu wanaosaka maji hayo kutoka kwenye maziwa, mito au vyanzo vingine vya mali asili.

Tamko la mtaalamu huyo limekuja baada ya bunge la Nigeria kupitisha mswaad wa sheria wa mazingira “Lagos environment Bill," wiki iliyopita , mswada ambao una vipengele vinavyofanya kuwa kosa la jinai kusaka maji kutoka katika vmali asili endapo watu hawajapatiwa rukhsa maalumu kutoka kwa serikali.

Ameongeza kuwa serikali ya Nigeria imeenda mbali sana kwa kutoza faini ambayo ni sawa na dola za Marekani 310 kwa watu wa kawaida wanaotafuta maji ili waweze kuishi, wakati kima cha chini cha mshahara nchini humo ni sawa na dola 60.