Sitegemei miujiza bali sote tuzungumze kwa nia njema- de Mistura
Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kwenye mzozo wa Syria, Staffan de Mistura amewataka wajumbe katika mazungumzo kuhusu mustakbali wa nchi hiyo kuweka mbele maslahi ya wananchi na kushirikiana ili hatimaye suluhu iweze kupatikana.
De Mistura amesema hayo mjini Geneva, Uswisi hii leo wakati akifungua awamu ya nne ya mazungumzo hayo yenye lengo la kumaliza vita nchini Syria iliyodumu kwa miaka sita sasa.
Amesema hategemei miujiza na anafahamu fika kuwa si kazi rahisi lakini washirikiane ili waweke msingi wa kuiweka Syria katika amani na umoja.
Bwana De Mistura amewaeleza wajumbe hao kutoka upande wa serikali na upinzani kuwa mazungumzo hayo ni fursa na wajibu wa kipekee na wasisahau kuwa mzozo huo umeweka kiza kwa kizazi kijacho cha Syria.
(Sauti ya de Mistura)
“Tunafahamu kitakachotokea iwapo tutashindwa tena. Vifo zaidi, machungu zaidi, ukatili zaidi, ugaidi zaidi na wakimbizi zaidi.”

Azimio hilo pamoja na mambo mengine linatoa wito wa kufanyika kwa uchaguzi huru na wa haki na wananchi wa Syria waamue wenyewe katiba yao.