Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Madai ya Libya kwamba wamesitisha mapigano hayajathibitishwa:Ban Ki-moon

Madai ya Libya kwamba wamesitisha mapigano hayajathibitishwa:Ban Ki-moon

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon leo amesema madai ya serikali ya Libya kwamba yatazingatia azimio la baraza la usalama la wiki hii linaloitaka nchi hiyo kusitisha mapigano mara moja na masbulizi dhidi ya raia bado hayajathibitishwa na hivi sasa hatua zinazochukuliwa na serikali haziko bayana.

Ban amewaambia waandishi wa habari mjini Paris Ufaransa ambako viongozi wa dunia wamekutana kujadili hali ya Libya kwamba usiku wa jana amezungumza kwa njia ya simu na waziri mkuu wa Libya Baghdad Mahmudi ambaye amesema utawala wa Libya utazingatia na kutekeleza azimio namba 1973.

Azimio hilo limeidhinisha kuchukuliwa kwa hatua ambazo ni za lazima kuwalinda raia dhidi ya mashambulizi ya majeshi ya serikali. Ban amesema waziri mkuu wa Libya

(SAUTI YA BAN KI-MOON)

Ameniomba kuingilia kati kuzuia hatua za kijeshi kwa upande wa jumuiya ya kimataifa , kusema kweli alisikika ana taharuki, haiku bayana wanafanya nini.Ametoa wito wa kufuatilia usitishaji mapigano. Madai ya Libya yanahitaji kuthibitishwa, hakuna shaka Walibya wanajaribu kuzuia hatua za kijeshi chini ya azimio 1973.

Ban ameongeza kuwa amezungumza mara kadhaa na waziri wa mambo ya nje wa Libya Musa Kousa akiitaka serikali kuacha ghasia na kusitisha mashambulizi mara moja. Kwa mujibu wa duru za habari majeshi ya Libya yameshambulia mji wa Mashariki wa Benghazi katika saa 24 zilizopita ambako ni makao makuu ya majeshi ya waasi, licha ya madai kwamba serikali imesitisha mapigano.Ban amesema

(SAUTI YA BAN KI-MOON)

Ukizingatia hali mbaya iliyoko mLibya ni muhimu kuendelea kuchukua hatua na maamuzi ya haraka, na Umoja wa Mataifa unashirikiana kwa karibu na mashirika ya kikanda na nchi wanachama kuchukua msimamo wa pamoja ,unaofaa, na kwa wakati kudhibiti hali.

Ban amesisitiza kwamba pamoja na kusitisha mara moja mapigano serikali ya Libya lazima iache kabisa kutuma vikosi vyake na kutumia silaha nzito kwenye miji mikubwa nchini humo ili watu waweze kuendelea na maisha yao ya kila siku bila kuwa na woga au hofu ya maisha yao.