BU lasisitiza wanawake washirikishwe kikamilifu katika ujenzi wa amani
Baraza la Usalama (BU) leo limefanyisha mkutano wa hadhara, wa siku nzima, ambao wawakilishi wa kimataifa 55 walizungumzia kuhusu suala la ‘Wanawake, Amani na Usalama\'.
Mkutano ulioongozwa na Naibu Waziri Mkuu wa Vietnam, ambaye taifa lake ndio linaloshika wadhifa wa mwenyekiti wa Baraza la Usalama kwa mwezi wa Oktoba. Baraza lilipitisha, kwa kauli moja, azimio liliolaani vikali ukiukaji wote wa sheria za kiutu za kimataifa zinazofungamana na hifadhi ya wanawake na watoto wa kike kwenye mazingira ya mapigano, na baada ya vita kusimamishwa. Miongoni mwa hatua za kuchukuliwa zilizopendekezwa na azimio ni ile inayomtaka KM aongeze idadi ya vyeo vya wanawake watakaoongoza taasisi za UM kwa niaba yake; na pia kuhakikisha nchi zote wanachama zinaripoti kwa Baraza la Usalama taarifa maalumu juu ya athari za hali ya mapigano na vurugu dhidi ya wanawake na watoto wa kike kwenye maeneo yao. Kwenye risala ya KM mbele ya wajumbe wa Baraza la Usalama, iliosomwa na NKM Asha-Rose Migiro, alisema hatua ya kuwashirikisha wanawake kwenye majadiliano ya kurudisha amani husaidia kuimarisha mapatano yanayokuwa na haiba inayoaminika, na huongeza fursa ya mapatano hayo kutekelezwa kwa mafanikio.