Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Fikra sahihi huja kwa lugha sahihi-UNESCO

Fikra sahihi huja kwa lugha sahihi-UNESCO

Tunaunga mkono lugha ya mama na matumizi ya lugha mbalimbali katika elimu, ndivyo unavyoanza ujumbe wa shirika hilo la Umoja wa Mataifa la elimu sayansi na utamaduni UNESCO, unaozungumzia siku ya kimataifa ya lugha ya mama inayoadhimishwa kila Februari 21.

Kauli mbiu ya mwaka huu ni Kuelekea mustakabali endelevu kupitia elimu kwa lugha mbalimbali, msisitizo ukiwa kuchochea maendeleo endelevu kupitia elimu kimataifa, kwa kutumia lugha ya mama na kwa lugha nyingine.

Katika kuadhimisha siku hii, UNESCO inatia shime matukio yanayohusisha lugha za mama, elimu kupitia lugha mbalimbali na katika makao makuu ya shirika hilo mjini Paris Ufaransa, shuguli hizo zinatarajiwa kutia fora.

Shirika hilo limesisitiza kwamba kuimudu lugha ya awali au ya mama huwezesha kupata ujuzi katika kusoma, kuandika na kuhesabu.

Siku ya kimataifa ya lugha ya mama inaunga mkono lengo namba nne la malengo ya maendeleo endelevu (SDGs) linalotaka uhakikisho kwa vijana wote na idadi kubwa ya watu wazima, wanaume na wanawake kufanikiwa katika kusoma na kuhesabu.