Uhaba wa chakula waathiri wakimbizi barani Afrika-WFP/UNHCR

Uhaba wa chakula waathiri wakimbizi barani Afrika-WFP/UNHCR

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani, WFP, Ertharin Cousin na Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR, Filippo Grandi wana wasiwasi mkubwa kutokana na uhaba wa msaada wa chakula utakaowaathiri wakimbizi takriban milioni 2 katika nchi 10 barani Afrika.

Kwenye taarifa yao ya pamoja wasema hali inaweza kuwa mbaya zaidi katika miezi ijayo endapo hakutapatikana fedha kukidhi mahitaji hayo ya chakula. Idadi ya wakimbizi barani Afrika imeongezeka kutoka milioni 2.6 mwaka 2011 hadi karibu milioni 5 mwaka 2016, na japokuwa fedha za wafadhili ziliongezeka katika kipindi hicho lakini hazilingani na mahitaji ya wakimbizi yaliopanda kwa kasi na hivyo kulazimu kupunguzwa kwa msaada wa chakula.

Katika nchi 10 barani Afrika msaada wa chakula kwa wakimbizi milioni 2 umepunguzwa ikiwemo Cameroon, Chad, Kenya, Mauritania, Sudan Kusini na Uganda. Huku bidhaa maalum zikipunguzwa Burkina Faso, Djibouti, Burundi na Ethiopia.