Skip to main content

Kutu ya ngano yasambaa Ulaya, Afrika na Asia ya Kati:FAO

Kutu ya ngano yasambaa Ulaya, Afrika na Asia ya Kati:FAO

Ugonjwa wa kutu ya ngano, ambao ni jamii ya fungus inayoweza kutokomeza mazao hadi asilimia 100 isipotibiwa kwenye ngano, imeendelea kusambaa barani Ulaya, Afrika na Asia ya Kati kwa mujibu wa tafiti mbili zilizotolewa na wanasayansi kwa ushirikiano wa shirika la chakula na kilimo FAO.

Ripoti hizo zilizochapishwa kwenye jarida la Nature baada ya kutolewa na chuo kikuu cha Aarhus na kituo cha kimataifa cha mahindi na uboreshaji wa ngano CIMMYTT, zinaonyesha mlipuko wa aina mpya ya maradhi hayo ambao ni kutu ya njano na kutu ya shina katika maeneo mengi duniani kwa mwaka 2016.

Na wakati huohuo utafiti umebaini kwamba aina ya kutu ya ngano iliyozoweleka pia imethibitishwa kusambaa katika nchi mpya zingine, na umesisitiza haja ya kubaini mapema na kuchukua hatua kudhibiti hasara kwenye uzalishaji wa ngano hasa katika bonde la Mediterranean.

FAO inasema ngano ni chakula muhimu kwa maisha ya watu zaidi ya bilioni moja katika nchi zinazoendelea, za Kaskazini na Mashariki mwa Afrika, Mashariki ya mbali na Magharibi, Kati na Kusini mwa Asia.