Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkakati mpana wahitajika kudhibiti kauli za chuki: Dieng

Mkakati mpana wahitajika kudhibiti kauli za chuki: Dieng

Harakati zozote za kudhibiti kauli chochezi na za chuki zinazoweza kusababisha migogoro zinahitaji mpango mpana unaojumuisha pande nyingi.

Hiyo ni kauli ya Adama Dieng, Mshauri maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu jinsi ya kuzuia mauaji ya kimbari, kauli ambayo ameitoa wakati wa mkutano wa kujadili suala hilo mjini New York, Marekani.

Dieng amesema hilo ni suala mtambuka ambalo sheria pekee haiwezi kusaidia kutokana na kuwepo kwa uhuru wa mtu kujieleza.

Hata hivyo amewaeleza washirika kuwa ni vyema kukawepo mizania ya uhuru wa kujieleza na umuhimu wa kuzuia au kupiga marufuku matukio yanayovuka mpaka ya kauli za chuki.

Dieng amesema mpango mpana uhakikishe sheria inakwenda pamoja na kutokomeza vyanzo vya chuki kama vile ubaguzi kwa misingi mbali mbali kama rangi na ihusishe mashauriano kati ya serikali na taasisi za kiraia.

Ametolea mfano Kenya ambako mwezi ujao kunafanyika uchaguzi mkuu na sasa kuna hatua mbali mbali zinazochukuliwa kuepusha kauli chochezi na za chuki ili kuepusha ghasia kama zilizojitokeza baada ya uchaguzi mkuu mwaka 2007