Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mwanasheria maarufu Myanmar auawa, UM wazungumza

Mwanasheria maarufu Myanmar auawa, UM wazungumza

Mtaalamu maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya haki za binadamu nchini Myanmar, Yanghee Lee, amelaani vikali mauaji ya kikatili ya mwanasheria mashuhuri wa kiislamu nchini humo, Ko Ni.

Taarifa ya ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa imesema Bwana Ko, ambaye ni mtaalamu wa sheria za kikatiba na pia mshauri wa kisheria wa chama cha National League for Democracy, NLD, aliuawa kwa kupigwa risasi nje ya uwanja wa ndege wa Yangon, siku ya Jumapili.

Bi. Lee ametoa wito kwa serikali ya Myanmar kulaani vikali tukio hilo hadharani na kuchunguza kitendo hicho kilichotokea wakati Bwana Ko akirejea kutoka Indonesia ambako alikuwa kwenye ujumbe wa serikali ulioshiriki ziara ya mafunzo kuhusu utangamano wa kidini.

Ingawa mshukiwa wa tukio hilo amekamatwa bado sababu za mauaji hayo hazijafahamika lakini mtaalamu huyo ametaka wananchi kujizuia kuchukua hatua zinazoweza kuchochea ghasia zaidi.

Bi. Lee ametuma rambirambi kwa familia ya mwanasheria huyo akisisitza kuwa kifo chake ni pengo kubwa kwa watetezi wa haki za binadamu Myanmar.