Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kutesa sio suluhisho na ni ukatili

Kutesa sio suluhisho na ni ukatili

Mtaalamu huru wa Umoja wa Mataifa kuhusu masuala ya mateso, Nils Melzer ametoa wito kwa Rais wa Marekani Donald Trump kufikiria upya kurejesha matumizi ya utesaji wa kuzamisha ndani ya maji na mbinu zingine za utesaji.

Amesema kama utawala huu mpya utafufua matumizi ya mbinu za kutesa, basi itakuwa janga kubwa kwani ulimwengu wote utafuata mkondo huo.

Ameongeza kuwa mbinu hizi ambazo hutumika kama mbinu za kuhoji, bila shaka zinaenda kinyume na sheria za kimataifa na kwa mantiki hiyo ametaja sababu tatu za kutokurejesha mbinu hizo.

Mosi amesema kutesa hakufanyi kazi, na ili kuondokana na maumivu makali na dhiki, muathirika atasema chochote kuondokana zahma hiyo na hivyo kupata ushahidi wa uongo na habari za kupotosha, pili, amesema hata kama inafanya kazi, haikubaliki kisheria au kimaadili, si ustaarabu na ni ukatili, ni unyama na hudhalilisha anaeteswa na mtesaji na jamii nzima na tatu amesema adhabu hizo zimepingwa na imekuwa ni marufuku katika mikataba ya Kimataifa ya Haki za Kiraia na Kisiasa na Mikataba ya Geneva.