Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Utawala wa sheria muhimu kujenga amani ya jamii:Ban

Utawala wa sheria muhimu kujenga amani ya jamii:Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa leo amesisitiza haja ya haraka ya kuimarisha utawala wa sheria duniani,akisema unaweza kusaidia kukabiliana na baadhi ya changamoto zinazoikabili jumuiya ya kimataifa hivi sasa.

Akizungumza katika mjadala wa siku moja kwenye baraza kuu la Umoja wa Mataifa Ban amesema mtu asiangalie popote bali vichwa vya habari kila siku ili kuthamini haja ya utawala wa sheria. Amesema katika ulimwengu wa Kiarabu watu kwa muda mrefu wamenyiwa uhuru na haki zao za msingi, na sasa wanataka haki, utu wao na utawala wa sheria.

Ameongeza kuwa Afrika, Asia na Ulaya wito unatolewa wa kuwepo utawala bora, uwazi, mapambano dhidi ya ufisadi, imani ya mfumo wa sheria, uwajibikaji kwa wahalifu na wanaokiuka haki za binadamu. Kilio chao ni kimoja amesema Ban, wanataka sio watu bali sheria kushika mkondo wake. Amesisitiza utawala wa sheria unawasilisha matumaini ya baadaye ya jamii nyingi.

Ameyataka mataifa yote duniani kutimiza ahadi waliyoitoa kwenye mkutano wa kimataifa wa 2005 kuwa watahakikisha utawala wa sheria unachukua mkondo kwa ajili ya faifa ya jamii zao.