UNMISS yapinga kukamatwa kwa mwandishi wake wa habari

26 Januari 2017

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, UNMISS umepinga kukamatwa, kuteswa na kunyanyaswa kwa mwandishi wa habari wa Radio ya Miraya ya Umoja wa Mataifa jijini Juba, Sudan Kusini.

UNMISS imesema mwandishi wa habari huyo pamoja na mfanyakazi wa Umoja wa Mataifa walikamatwa na wanajeshi wa SPLA, na kuwekwa kizuizini kwa muda wa saa tano, wakati akiandaa habari ndani ya makumbusho ya John Garang.

Msemaji wa UNMISS Daniel Dickinson amesema ujumbe huo umewasiliana na Wizara ya Mambo ya Nje kuhusu tukio hilo, na kutoa wito kwa wadau kufanya uchunguzi wa haraka na kuwaleta wahusika mbele ya sheria, na akakumbusha kile kilichomo ndani ya mkataba wa SOFA baina ya UNMISS na serikali ya Sudan Kusini ..

(Sauti ya Daniel)

"Usalama, ulinzi na uhuru wa kutembea wa wafanyakazi wa UNMISS ni lazima uhakikishwe, hususan wakati wanatekeleza majukumu yao rasmi, kama ilivyokuwa hapa. Kukamatwa kwa mfanyakazi bila ya kumpeleka kwa mwakilishi wa karibu zaidi wa UNMISS, bila shaka pamoja na ushahidi sahihi, ni ukiukaji wa mkataba huo."

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter