Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Si lazima kwenda nje ya nchi kutimiza ndoto zako

Picha: IOM/Video capture
Alain, Mkimbizi mjasiriamali aliyejitolea kurudi nyumbani toka uhamiaji Libya.

Si lazima kwenda nje ya nchi kutimiza ndoto zako

Wahamiaji waliorejea nyumbani kwa hiari baada ya mateso nchini Libya na Niger wameamua kujihusisha na shughuli za kiuchumi ili kuboresha maisha yao. Selina Jerobon na ripoti kamili.

(Taarifa ya Selina Jerobon)

Hatua hiyo imewezekana kufuatia miradi iliyoanzishwa na shirika la uhamiaji la Umoja wa Mataifa, IOM ikilenga kuimarisha mitandao ya wahamiaji hayo kijamii, kiweledi,kiuchumi na hata kibinadamu na hivyo kuepusha fikra za baadaye za kukimbia nchi hiyo.

Miongoni mwao Alain fundi mwashi raia wa Cameroon ambaye baada ya kurejea nyumbani akitokea Niger amewezeshwa kufungua kiwanda kidogo cha kutengeneza makasha ya bati yanayotumiwa na polisi au wanajeshi kusafirishia mizigo.

(Sauti ya Alain)

“Niliondoka kwa sababu nilikuwa na mradi wenye lengo la kuboresha zaidi mambo ambayo nilikuwa nafanya hapa nyumbani, kwa sababu hapa mambo yanafanyika kizamani. Iwapo una ndoto si lazima unaweza kutimiza nje ya nchi, hata ndani ya nchi yako inaweza kutimia.”

Naye Sedi raia wa Guinea Bissau baada ya kurejea nyumbani amepatiwa stadi za kuendesha biashara ambapo amefungua duka la bidhaa ndogondogo.

(Sauti ya Sedi)

“Wakati wa mafunzo tumefundishwa jinsi ya kusimamia rasilimali pamoja na biashara.”

IOM inasema wahamiaji wote wanaorejea nyumbani wana haki ya kupatiwa usaidizi kupitia miradi hiyo ambayo inawezekana kufuatia usaidizi wa Muungano wa Ulaya.