Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sekta mbili kupigwa jeki kufuatia mradi wa dola milioni 50- Cuba

Sekta mbili kupigwa jeki kufuatia mradi wa dola milioni 50- Cuba

Kukuza ukuaji endelevu wa sekta ya mifugo ili kuongeza mapato na kutoa nafasi za ajira kwa familia katika vyama vya ushirika  ndio lengo la mkataba wa kifedha uliwekwa saini leo kati ya Shirika la kimataifa la ufadhili wa maendeleo ya kilimo IFAD na serikali ya Cuba.

Makubaliano hayo ya ushirika wa maendeleo wa mradi wa mifugo ukanda wa Mashariki na kati (PRODEGAN) yalisainiwa huko Roma Italia na Mkuu wa IFAD Kanayo Nwanze na Balozi wa Cuba nchini Italia ambaye pia ni mwakilishi wa kudumu wa mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini humo Alba Beatriz Soto Pimentel,

Kwa mujibu wa taarifa kutoka IFAD, gharama ya jumla ya mradi huo ni dola milioni 50 ambapo  IFAD itakopesha dola milioni 11.9, shirika la kifaransa la maendeleo AFD litatoa dola milioni 28.1 na zilizosalia dola milioni 10 zitatoka kwa serikali ya Cuba.

Meneja wa IFAD nchini Cuba Lars Anwandter amesema  shirika lake linaweza kusaidia juhudi muhimu za kuleta mabadiliko ya sekta ya kilimo kwa kusaidia wakulima wadogo kupitia vyama vya ushirika binafsi inayowakilisha uti wa mgongo wa sekta za uzalishaji. 

PRODEGAN itashughulikia kubadili msimamo na kusaidia vyama vya ushirika na wakulima wadogo kuongeza utengenezaji na uuzaji wa maziwa na nyama na kuweka msisitizo maalum juu ya uwezeshaji wa wanawake na vijana.

Familia 11,500 zitafaidika  katika vyama 105 vya ushirika, na kufikia jumla ya walengwa 34,500 katika jimbo la Camagüey manispaa ya Guáimaro, Sibanicú, Camagüey na Jimaguayú. Tangu mwaka 1980 IFAD imesaidia mipango ya maendeleo vijijini kwa gharama ya jumla ya dola milioni 117, ikiwa ni pamoja usaidizi wa moja kwa moja wa uwekezaji wa dola milioni 37.