Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watendaji wa UM wawasili Aleppo, uhamishaji raia warejea

Watendaji wa UM wawasili Aleppo, uhamishaji raia warejea

Kazi ya kuondoa raia kutoka Aleppo nchini Syria ambako mapigano yameshika kasi, imeanza tena baada ya kusitishwa kwa zaidi ya siku moja huku watendaji 20 wa Umoja wa Mataifa wakiwasili eneo hilo kuhakikisha uhamaji wao unakuwa salama.

Hatua hiyo imekuja baada ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kupitisha azimio siku ya Jumatatu lililoridhia kupelekwa kwa watendaji  hao wa Umoja wa Mataifa.

Naibu Msemaji wa Umoja wa Mataifa Farhan Haq amewaambia waandishi wa habari mjini New York, Marekani kuwa kazi ya kuondoa raia hai kutoka maeneo yaliyozingirwa itaendelea hadi baadaye leo jumatano kwa saa za Syria.

"Takribani wafanyakazi 20 kutoka Damascus wamepelekwa Aleppo kusaidia kazi ya kufuatilia uhamishaji wa raia na majukumu mengine kwenye mji huo. Timu ya Umoja wa Mataifa imeendelea kuwepo kwenye kituo cha ukaguzi cha serikali kilichopo Ramouseh huko Aleppo tangu tarehe 15 mwezi huu. Hofu kubwa ni ulinzi wa raia kutoka maeneo haya. Mchakato wa kuwahamisha bado unatisha, huku watu wengi walio hatarini zaidi wakiwa wamelundikana wakisubiri kwa muda mrefu kwenye mazingira ya baridi kupindukia.”

Shirika la afya duniani WHO limesema waliosafirishwa hadi Uturuki kwa matibabu ni pamoja na watu 301 wakiwemo majeruhi na wagonjwa ambapo kati yao 93 wako kwenye hali mbaya.

Wakati huo huo hii leo Baraza la Usalama limepitisha azimio linaloendeleza ufikishaji wake misaada ya kibinadamu huko Syria kwa miezi 12 zaidi.  Azimio hilo linataka serikali ya Syria kuruhusu misaada hiyo kwa raia ifikishwe haraka.