Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hakuna mikono salama kwa silaha za maangamizi- Eliasson

Hakuna mikono salama kwa silaha za maangamizi- Eliasson

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa leo limekuwa na mjadala wa wazi kuhusu azimio namba 1540 la  kuzuia janga lisababishwalo na matumizi ya kiholela ya silaha za maangamizi ya umma.

Mjadala huo umejikita kwenye mfumo wa Umoja wa Mataifa katika  kuzuia matumizi ya kiholela ya silaha hizo kunakofanywa na vikundi visivyo vya kiserikali, teknolojia mpya na vitisho vipya katika suala hilo.

Akizungumza katika mjadala huo, Naibu Katibu Mkuu wa UM Jan Eliasson amesema vitisho vya matumizi ya silaha hizo ni kwa jamii nzima ya kimataifa hivyo Baraza la Usalama lina wajibu wa kuhakikisha kuwa wamiliki wa silaha hizo wanawajibishwa kwa kuwa..

(Sauti ya Eliasson)

“Hakuna mikono salama kwa silaha mbaya. Na silaha za maangamizi ya umma kwa ujumla ni mbaya. Kuna njia moja tu ya kuepusha magaidi kupata silaha hizo za maangamizi ya umma na njia hiyo ni kwa kuzipiga kabisa marufuku.”

Awali Baraza hilo lilipitisha azimio namba 2325 ambalo pamoja na mambo mengine linaweka msisitizo kwa nchi kuimarisha jitihada kwenye kutekeleza azimio namba 1540 la mwaka 2004 linalozuia kuenea kwa silaha za maangamizi ya umma.