Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto wamezoea milio ya makombora Syria

Watoto wamezoea milio ya makombora Syria

Zaidi ya watu milioni Tano huko Syria wanapata usaidizi wa kibinadamu kila mwezi huku wengine milioni Saba wakipatiwa matibabu kutokana na mapigano yanayoendelea nchini humo.

Hiyo ni kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa ambapo akizungumza hii leo huko Vienna, Austria, Katibu Mkuu Ban Ki-moon amesema kundi hilo ni baadhi ya tu, ilhali kazi kubwa sasa ni kufikia wengine walionasa kwenye mapigano huko Aleppo.

(Sauti ya Ban)

"Tulichoshuhudia  hivi karibuni huko Mashariki mwa Aleppo kinaumiza sana moyo. Tumekuwa tunajaribu sana kupeleka misaada ya kuokoa maisha na kujikwamua kwa watu walionasa katikati ya mapigano na maeneo mengine yasiyofikika. Imekuwa ni kazi ngumu sana wakati huu ambapo vita inaendelea.”

 Wakati huo  huo, mwakilishi wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF n chini Syria Hanaa Singer amezungumzia kile alichoshuhudia wakati wa ziara yake nchini humo akisema milio ya risasi na makombora yanaweza hata kusababisha uziwi.

Hata hivyo amesema watoto walikuwa wakicheka vile ambavyo alikuwa akistuka kadri milio ya makombora ilivyokuwa inasikika, ikiwa ni jambo la kawaida kwao ingawa halipaswi kuwa hivyo.