Azimio la Dubai lasongesha nafasi ya anga ya juu kwa maendeleo

Azimio la Dubai lasongesha nafasi ya anga ya juu kwa maendeleo

Mkutano wa ngazi ya juu kuhusu jinsi sayansi na teknolojia ya anga za juu vinaweza kuchagiza maendeleo na kudhibiti mabadiliko ya tabianchi, umefika tamati huko Dubai, Falme za kiarabu kwa kupitisha azimio.

Azimio hilo pamoja na mambo mengine linafungua njia zaidi za kutumia Nyanja ya anga za juu kwa manufaa zaidi ya maendeleo endelevu.

Kupitia azimio hilo pia, washiriki wa mkutano huo wa siku tano kutoka serikali, mashirika ya kimataifa na taasisi za elimu wamesisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa katika masuala ya anga za juu.

Simonetta Di Pippo ni mkurugenzi wa ofisi ya Umoja wa Mataifa kuhusu masuala ya anga za juu, UNOOSA ambao ndio waandaji wa mkutano huo

(Sauti ya Simonetta)

 “Hapa Dubai kwa pamoja tumeandaa mapendekezo ya kushughulikia masuala muhimu wa maendeleo ndani na nje ya anga za juu. Mathalani ujumuishi wa teknolojia mpya na miundo mipya ya biashara inayoathiri shughuli zetu za anga a juu. Azimio la Dubai pamoja na kile tulichojifunza kwenye mkutano huu vimetupatia uelewa wa jinsi ya kusonga mbele katika kutumia anga za juu kwa maendeleo na pia umuhimu wa kupata fursa zaidi kwenye anga za juu kwenye nchi nyingi, halikadhalika kusaidia nchi kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu.”

Mkutano huo wa Dubai ulikuwa wa kwanza kati ya mikutano mitatu kuelekea maadhimisho ya miaka 50 ya mkutano wa kwanza kabisa wa Umoja wa Mataifa kuhusu matumizi ya anga za juu kwa amani, UNISPACE.

Maadhimisho ya miaka 50 ya UNISPACE yatafanyika mwezi Juni mwaka 2018.