Skip to main content

Radio Eye Sudan Kusini yafungwa, Adama apaza sauti

Radio Eye Sudan Kusini yafungwa, Adama apaza sauti

Mshauri maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu kuzuia mauaji ya kimbari Adama Dieng, amehitimisha ziara yake ya siku tano nchini  Sudan Kusini akisema kuwa kile kilichoanza nchini humo kama mzozo wa kisiasa, taratibu kinageuka kuwa mzozo wa kikabila.

Taarifa iliyotolewa mjini Juba, imemnukuu Bwana Dieng  akisema kuwa mazungumzo yake na pande mbali mbali nchini humo ikiwemo serikali na mashirika ya kiraia, yamethibitisha hofu yake ya mzozo huo kupanuka kwa misingi ya kikabila na hatimaye mauaji ya kimbari.

Amesema badala ya harakati za kuimarisha utaifa wa Sudan Kusini,  kinachofanyika sasa ni kujenga mgawanyiko mkubwa kwa misingi ya kikabila, jambo ambalo amesema lilikuwa chanzo cha ghasia za mwezi Julai mwaka huu.

Halikadhalika amezungumzia kitendo cha kufungwa kwa kituo cha Radio Eye mjini Juba…

(Sauti ya Adama)

“Kama unaniambia kuwa hii radio ilikuwa inaeneza ujumbe wa amani, walichotakiwa wao kufanya ni kuwatia moyo na kuwapongeza, na kutumia radio hiyo kama mfano na kusema kuwa huo ndio ujumbe tunaotaka, kwani hilo ndio jambo nimekuwa naeleza mamlaka. Nilikuwa sifahamu hili, na kabla ya kuondoka nchi hii nitaandikia barua mamlaka husika ili wafikirie upya uamuzi wao , kwani huu ni wakati tunahitaji chombo cha kutuma ujumbe thabiti wa amani.”

Amesisitiza kuwa mauaji ya kimbari ni mchakato, kwa kuwa hayatokei ghafla na hivyo ni lazima yaepushwe Sudan Kusini.