Mediteranea "yameza" watoto na wajawazito- UNICEF

Mediteranea "yameza" watoto na wajawazito- UNICEF

Watoto na wanawake wajawazito ni miongoni mwa watu 240 waliokufa maji mwambao wa Libya Jumatano wiki hii wakijaribu kuingia Ulaya kwa boti. Taarifa ya Assumpta Massoi.

(TAARIFA YA ASSUMPTA)

Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF mwanamke mmoja kutoka Liberia, miongoni mwa watu 29 walionusurika amesema amepoteza mtoto wake mwenye umri wa miaka miwili, binti wa miaka 13 na kaka yake wa miaka 21.

Helena Rodrigues daktari mtaalamu wa masuala ya wanawake wa UNICEF amesema zahma hiyo ni machungu makubwa yanayoleta msongo wa mawazo na madhila mengine, na anashirikiana na wahudumu wa afya wa Italiakuwatibu manusura akiwemo mama huyo kutoka Liberia anayesumbuliwa na kichomi.

Manusura wamesema walilipa maelfu ya dola kuvuka bahari ya Mediteranea kutokea Libya lakini walipoiona boti waligoma kuingia na ndipo wasafirishaji haramu walipowafyatulia risasi wakiwashinikiza kwenda, na hii ndio sababu watu wengi sana wamezama baada ya boti kuzidiwa uzito.

Wahanga wengi wa mkasa huo ni kutoka Senegal, Liberia, Guinea, na Nigeria.