Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

ISIL yaendelea kufurusha watu kwa nguvu Iraq: UM

ISIL yaendelea kufurusha watu kwa nguvu Iraq: UM

Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa imesema imepokea ripoti kwamba kundi la kigaidi la ISIL limeendelea kuwafurusha na kuwahamisha watu kwa nguvu katika siku chache zilizopita.

Watu 1600 waliondolewa kutoka Hamam al-Alil na kupelekwa mji wa Tal Afar , huku baadhi ya familia zikijulishwa kuwa zitapelekwa Syria.

Kamishna mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa, Zeid Raa'd Al Hussein amesema mwenendo huo unawatia hofu na kwamba ISIL itazitumia familia hizo kama ngao wakati makombora yakirushwa.

Ofisi hiyo imesema imeendelea pia kupokea taarifa za mauaji ya watu wengi ikiwemo ya Jumatatu ambapo ISIL iliuwa wapiganaji wake 50 kwa madai ya kulitelekeza kundi hilo, huku Jumatano kukiwa na taarifa za mauaji ya watu zaidi ya 300 ambazo bado zinachunguzwa.

Watu pia wameendelea kutekwa ,Ravina Shamdasani ni msemaji wa ofisi ya haki za binadamu

(SAUTI YA RAVINA)

“Tuna taarifa kwamba wanamgambo wa ISIL wanawashikilia mateka wanawake karibu 400 kutoka Kurdi jamii za Wayazidi au waislamu wa Shia mjini Tal Afar. Tangu Oktoba 17 ISIL imearifiwa pia kuwaingiza kwa nguvu watoto vitani wenye umri w  a miaka 9 au 10 ili kupigana Mosul. “