Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maandamano nchini CAR yaleta tafrani

Maandamano nchini CAR yaleta tafrani

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati ,MINUSCA imeripoti migogoro na machafuko katika mji mkuu Bangui, kufuatia maandamano dhidi ya ujumbe huo pamoja na serikali ya nchi hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini New York leo, msemaji wa katibu mkuu Stephan Dujarric amesema MINUSCA imeripoti milio ya risasi na uporaji katika sehemu kadhaa jijini humo.

(Sauti ya Dujarric)

" Ripoti ambazo hazijathibitishwa zimesema kuna majeruhi na kwa mujibu wa ripoti nyingine ya awali, walinda amani wanne wa Umoja wa Mataifa wamejeruhiwa. Kikosi cha ulinzi cha serikali na walinda amani wamepelekwa katika maandamano ili kurejesha utulivu."

Amesema MINUSCA imeimarisha doria katika mji mkuu wa Bangui ili kuhakikisha usalama kwa raia, na itaendelea kufuatilia hali hiyo kwa ukaribu zaidi.

Na kwa mantiki hiyo amesema Umoja wa Mataifa itaendelea kusimama na serikali na wananchi wa nchi hiyo kwa mujibu wa mamlaka iliyopewa.