Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto Haiti wamo hatarini kunyanyaswa

Watoto Haiti wamo hatarini kunyanyaswa

"Tunatumai kheri lakini tunajiandaa na hali mbaya zaidi". Hayo ni kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto(UNICEF) kuhusu dhoruba ya kimbunga Matthew iliyoleta uharibifu mkubwa na madhila mengi hususan Kusini mwa Haiti.

UNICEF imesema hali halisi katika maeneo yaliyoathirika mno ya Grande Anse na Grande South ambapo takriban watoto 500,000 wanaishi haijulikani, na kuna uharibifu mkubwa wa miundombinu na barabara na hii inasababisha kazi za tathmini na usafirishaji wa misaada kuwa ngumu.

Vile vile, shirika hilo limesema liko mbioni kuhakikisha watoto katika maeneo hayo wapo katika hali ya usalama. Christophe Boulierac ni Msemaji wa UNICEF, Geneva...

(Sauti ya Chrisophe)

"Eneo moja lililoathirika zaidi, ni eneo ambalo kuna watoto wengi wanaohitaji ulinzi, na ni jambo lenye kutia wasiwasi, kwa sababu wamo hatarini zaidi kunyanyaswa na kutumiwa vibaya, na hili ni tatizo kubwa Haiti".

Wakati huo huo, UNICEF ikishirikiana na serikali ya Haiti, imeandaa vifaa vya dharura kuwafikia hadi watu 10,000, ikiwa ni pamoja na vifaa vya kusafisha maji na mazingira, na limesema mahitaji mengine ya kibinadamu yatahitajika pindi tathmini ya hali halisi itakapokamilika.