Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNICEF yaitaka Zimbabwe ilinde watoto dhidi ya madhara ya kisiasa

UNICEF yaitaka Zimbabwe ilinde watoto dhidi ya madhara ya kisiasa

Shirika la kuhudumiwa watoto duniani, UNICEF limeitaka Zimbabwe kulinda watoto wakati taifa hilo linaelekea katika kupiga kura ya maoni kuhusu katiba na uchaguzi mkuu baadaye mwaka huu.

Katika ziara yake ya siku mbili nchini humo Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF Anthony Lake pamoja na kuitakia amani Zimbabwe katika shughuli hizo, amesema ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha wanawake na watoto hawakumbwi na ghasia wakati wa mchakato wa kura ya maoni kuhusu katiba tarehe 16 mwezi huu na hata wakati wa uchaguzi mkuu.

Amesema nyakati za wasiwasi kama vile wakati wa chaguzi, ni vyema kaya, shule na jamii zikawa pahala salama na kwamba watoto ni lazima watoto wahakikishiwe hawakumbani na usumbufu wowote ule katika kupata mahitaji muhimu ya kijamii. Amesema watoto sio wanasiasa na hivyo hawapaswi kukumbwa na kashikashi za kisiasa.

Halikadhalika Bwana Lake katika ziara yake hiyo amekutana na Waziri Mkuu wa Zimbabwe Morgan Tsvangirai na Waziri wa mambo ya nje Nicholas Goche ambapo walimhakikishia kuwa watasimamia ulinzi wa mtoto.

Bwana Lake alitembelea kituo cha afya na shule nchini humo ambavyo vimepatiwa misaada ya dawa na vitabu vya kiada.