Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wasichana wanatumia saa milioni 160 zaidi kufanya kazi za nyumbani:UNICEF

Wasichana wanatumia saa milioni 160 zaidi kufanya kazi za nyumbani:UNICEF

Wasichana wa umri wa kati ya miaka 5 na 14 wanatumia asilimia 40 zaidi ya muda au saa milioni 160 kwa siku kufanya kazi za nyumbani zisizo na malipo kote duniani. Taarifa kamili na Assumpta Massoi.

(Taarifa ya Assumpta)

Kazi hizo ni pamoja na kuteka maji na kusenya kuni, ikilinganishwa na wavulana , imesema ripoti ya shirika la Umoja wa mataifa la kuhudumia watoto UNICEF iliyotolewa leo, kabla ya siku ya kimataifa ya mtoto wa kike itakayoadhimishwa Jumanne ijayo Oktoba 11.

Ripoti hiyo “Kuimarisha Uwezo wa Takwimu kwa ajili ya Wasichana: Kuorodhesha idadai na kuangalia mbele kwa ajili ya ajenda ya 2030, inajumuisha makadirio ya kwanza ya dunia ya wakati ambao wasichana wanatumia kufanya kazi za nyumbani kama vile kupika, kusafisha, kutunza familia, kuteka maji na kusenya kuni.

Ripoti inaonyesha kwamba tofauti hiyo huanza mapema na mara nyingi kazi zinazofanywa na mtoto wa kike hazionekani na hazithaminiwi.

Maeneo yaliyoathirika zaidi ni pamoja na Somalia, Burkina Faso na Yemen, huku utafiti ukitaja kuwa wasichana wa miaka 10 na 14 Kusini mwa Asia, Mashariki ya Katyi na Afrika ya Kaskazini hutumia muda mara mbili kufanya kazi za nyumbani kuliko wavulana.

Mwandishi wa ripoti hiyo Claudia Cappa wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEFanasema,

(Sauti ya Claudia)

"Kutofautiana kwa hizi kazi za nyumbani inaonyesha kwamba jukumu la msingi la mtoto wa kike ni kuwa nyumbani na kufanya kazi hizo. Na hii inawafanya kutojitegemea kiuchumi."

Na Bi Claudia anapendekeza kuwa..

(Sauti ya Claudia)

"Ni muhimu kwamba sisi tunawekeza kwa wasichana katika uwezo wao na kuhakikisha kwamba wanakua kwa kujiamini nakujihisi kuwa na nguvu katika maisha yao. Na ni muhimu pia kuziimarisha jamii na familia ili kuwapa msaada muhimu wa kuwasaidia wasichana."