Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Guterres apendekezwa rasmi na Baraza la Usalama kuwa Katibu Mkuu UM

Guterres apendekezwa rasmi na Baraza la Usalama kuwa Katibu Mkuu UM

Hatimaye mchakato wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa la kumpata Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa umefikia ukingoni hii leo baada ya baraza hilo kupitisha kwa kauli moja azimio nambari 2322 la mwaka 2016 la pendekezo la kuridhia Antonio Guterres wa Ureno kuwa Katibu Mkuu wa Tisa wa chombo hicho. Assumpta Massoi na taarifa zaidi.

(Taarifa ya Assumpta)

Mchakato ulioleta wagombea 13 ambapo baada ya kura sita zisizo rasmi za Baraza la Usalama ikiwemo ile inayoonyesha tofauti za kura na Guterres aling’ara zaidi na ndipo baraza liliandaa azimio la kuamua kumpitisha, azimio lililopigiwa kura leo katika kikao cha siri.

Balozi Vitaly Churkin wa Urusi ambaye ni Rais wa Baraza la Usalama kwa mwezi Oktoba akawaeleza wanahabari..

(Sauti ya Churkin)

“Baraza la usalama limepitisha kwa kauli moja azimio lifuatalo..Baraza la Usalama baada ya kuzingatia hoja ya mapendekezo ya uteuzi wa katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, linapendekeza kwa Baraza Kuu kuwa Antonio Guterres ateuliwe kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.”

Aliulizwa nini ujumbe wa Baraza hilo kwa mamilioni ya wanawake ambao waliamini kuwa huu ni wakati wao kushika wadhifa huo.?

image
Rais wa Baraza la Usalama Balozi Vitaly Churkin (kushoto) akikabidhi maamuzi ya baraza kwa Rais wa Baraza Kuu Peter Thomson (kulia) hii leo. (Picha:UN/Amanda Voisard)
(Sauti ya Churkin)

"Tulikuwa na mchakato wa wazi na tulikuwa na asilimia 50 ya wagombea wanawake, lakini hatimaye kulikuwa na makubaliano baina ya wanachama kuwa mgombea aliyekidhi zaidi vigezo ni Antonio Guterres.”

Na sasa kwa mujibu wa Ibara ya 97 ya katiba ya Umoja wa Mataifa jina lake linapelekwa Baraza Kuu kwa ajili ya kupitishwa ambapo ripoti zinasema kuwa Baraza hilo litakutana alhamisi ya tarehe 13 mwezi huu wa Oktoba.