Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kukabiliana na athari za vita kwa wakimbizi ni wajibu wa kila mtu:Ban

Kukabiliana na athari za vita kwa wakimbizi ni wajibu wa kila mtu:Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema iwe mtu amepitia athari za vita ama la, dunia ina wajibu wa kukabiliana na hali halisi ya wakimbizi na athari za vita.

Akizungumza kwenye mkutano wa kamati ya utendaji ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR, mjini Geneva, amesema watoto waliojeruhiwa wanalengwa hospitalini, sambamba na wahudumu wa afya ambao wangeweza kuokoa maisha yao.

Ban ameongeza kuwa silaha za uharibifu zimekuwa zikitumika zaidi na zaidi dhidi ya raia, kwa makusudi uhalifu wa vita unatekelezwa

(SAUTI YA BAN)

“Upuuzaji wa makusudi na wa wazi wa sheria za kimataifa unasababisha kwa kiasi kikubwa mateso na uharibifu wa muda mrefu. Tunahitaji nchi kuvuka wigo wa maslahi yao ya kitaifa na kuja pamoja kwa nguvu zote katika, mwitikio wa kimataifa.”

Amesema idadi ya wakimbizi na wakimbizi wa ndani ni kubwa sana na kila mmoja anawasilisha uhai, lakini akaonya kwamba haya sio madhila ya idadi, bali ni madhila yanayohitaji mshimakano.