Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Licha ya mkwamo siwezi itelekeza Syria- de Mistura

Licha ya mkwamo siwezi itelekeza Syria- de Mistura

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo limekuwa na kikao cha dharura kuhusu Syria kufuatia mashambulizi ya Ijumaa na Jumamosi huko Aleppo yaliyosababisha vifo, majeruhi na huduma za msingi kama vile maji kukatwa.

Akihutubia kikao hicho, mjumbe maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa Syria, Staffan de Mistura amesema hali ni mbaya huko Aleppo, misafara ya huduma za msingi ikishindwa kuingia kutokana na ukosefu wa hakikisho la usalama.

Bwana de Mistura amesema karibu miaka sita sasa ya mzozo wa Syria, makubaliano ya kusitisha mapigan hayazingatiwi hivyo akawasilisha ombi lake kwa Baraza….

“Chondechonde wekeni mwelekeo wa hatua za pamoja ili kuimarisha sitisho la mapigano nchini Syria.Bado ninashawishika kuwa tunaweza kubadili mwelekeo. Tumewezesha kuthibitisha hilo siku za nyuma. Tumepita safari ndefu sana, tusishindwe kuruhusu makubaliano ya sitisho la mapigano yatwame na yafukiwe kwenye vumbi la Aleppo”

Bwana de Mistura amesema mara kwa mara anaulizwa kwa nini asijiuzulu kutokana na mkwamo katika suluhu ya mzozo wa Syria?

Kwa kweli kwa kufanya hivyo, haitasaidia chochote na badala yake itatuma ujumbe thabiti kuwa jamii ya kimataifa imeitelekeza Syria, na hatutaiacha Syria peke yake,na nanyi pia msiitelekeze.”