Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ziara ya baraza la usalama imeondoa shaka na shuku- Moghae

Ziara ya baraza la usalama imeondoa shaka na shuku- Moghae

Mwenyekiti wa tume ya pamoja ya kufuatilia na kutathmini makubaliano ya amani Sudan Kusini, JMEC, Festus Moghae amesema ziara ya wajumbe wa baraza la usalama nchini humo iliyomalizika jumapili ni kielelezo kuwa jamii ya kimataifa inasaka amani ya kudumu nchini humo.

Akizungumza kwenye mji mkuu wa Sudan Kusini, Juba, Bwana Moghae amesema ziara hiyo pia imesaidia kumaliza shuku kwa upande wa serikali juu ya uamuzi wa Umoja wa Mataifa wa kuridhia kikosi cha kikanda cha ulinzi wa amani.

(Sauti ya Moghae)

“Serikali wa upande wake ilikuwa inasita, kwa sababu ilihisi kuwa kupelekwa kwa kikosi ni kama uvamizi unaokiuka mamlaka ya nchi hiyo. Sisi tulilazimika kueleza kwa kadri ya uwezo wetu kuwa si kwa mantiki hiyo kwa kuwa kikosi hicho kitafanya kazi kwa ushirikiano na serikali.”

Tayari Sudan Kusini imekubali kupelekwa kwa kikosi hicho kitakachokuwa na askari 4,000 kutoka nchi za ukanda huo wa Afrika ambapo Bwana Moghae amesema kuwa..

 “Kikosi hicho kinachozungumziwa si kingine bali ni kikosi cha ulinzi, ulinzi wa raia katika kila neno lake, ikiwemo taasisi nyeti ambazo ni muhimu kwa taifa na kila mtu hapa.”