Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mtandao wa mashambulizi ya albino Msumbiji bado ni siri- Ero

Mtandao wa mashambulizi ya albino Msumbiji bado ni siri- Ero

Nchini Msumbiji, hali ya watu wenye ulemavu wa ngozi, albino bado ni ya mashaka na hofu kubwa kutokana na kwamba vinara wa mashambulizi dhidi yao bado hawajafahamika na mtandao wao ni kama ule wa madawa ya kulevya.

Amesema mtaalam huru wa Umoja wa Mataifa kuhusu watu wenye ulemavu wa ngozi, albino Ikponwosa Ero baada ya kuhitimisha ziara yake nchini Msumbiji.

Bi. Ero amesema yadaiwa kuwa vinara wa mashambulizi wanatoka nje ya Msumbiji lakini hadi sasa hakuna uthibitisho wowote wa madai hayo wakati huu ambapo hakuna yeyote aliyewahi kukamatwa na kushtakiwa.

Akiwa Msumbiji alitembelea maeneo ya Beira, Nampula hadi Maputo akakutana na albino na familia zao akisema wana hofu tangu wanapozaliwa hadi kaburini kwa kuwa siyo tu viungo na nywele zao zinasakwa, bali hata vinyesi vyao.

Hata hivyo amepongeza Msumbiji kwa hatua iliyochukua za kuimarisha ulinzi lakini ametaka kazi zaidi ili kutekeleza mpango wa Afrika wa kulinda albino.