Tunataka kuona ushirikiano zaidi na Sudan Kusini yanachochea mzozo- Baraza

Tunataka kuona ushirikiano zaidi na Sudan Kusini yanachochea mzozo- Baraza

Wajumbe wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa wamewasili Juba, Sudan Kusini tayari kwa ziara ya siku tatu nchini humo.

Msafara huo unaongozwa na Marekani na Senegal katika ziara ambayo wajumbe hao watatathmini kile kinachoelezwa kuwa ni janga la kibinadamu la kusikitisha.

Samantha Power ni mwakilishi wa kudumu wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa na amezungumza na wanahabari baada ya kuwasili Juba.

(Sauti ya Samantha)

“Tuko hapa, bahati mbaya si kwa fikra za bashasha, bali kutokana na wasiwasi wetu kuhusu mapigano ambayo yamezidi kuzorotesha hali ya usalama na pia kuongeza hali mbaya ya kibinadamu kwa raia wa nchi hii.

Wakisaka ushirikiano kati ya Umoja wa Mataifa na serikali ya mpito Sudan Kusini, Bi. Power amesem serikali inashindwa kushirikiana na chombo hicho.

(Sauti ya Samantha)

“Mara kwa mara baraza limepokea ripoti za kusikitisha za vikwazo vinavyowekwa ili kukwamisha utendaji wa UNMISS na watoa huduma za misaada. Huu ni ujumbe ambao tutafikisha kwa pande zote tutakazokutana nazo ikiwemo serikali. Ni muhimu sana kuacha Umoja wa Mataifa  ufanye kazi zake.”

Pamoja na kuongeza muda wa UNMISS, baraza la usalama pia liliridhia kupelekwa kwa kikosi cha kimataifa ambacho kimeruhusiwa kutumia nguvu kulinda mali za Umoja wa Mataifa, raia, na wafanyakazi.