Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Bei duni ya mafuta yaathiri ukuaji wa sekta ya madini- UNIDO

Bei duni ya mafuta yaathiri ukuaji wa sekta ya madini- UNIDO

Ripoti mpya ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya viwanda (UNIDO), imesema kuwa ukuaji wa uchumi duniani kutokana na sekta ya uchimbaji madini ulikuwa mdogo mwaka 2015, ukiwa umeathiriwa na bei ndogo ya mafuta ambayo hayajasafishwa.

Ripoti hiyo ya kila mwaka inayotoa takwimu za kimataifa kuhusu uchimbaji madini, imeonyesha kuwa uzalishaji wa madini ulipanda kwa asilimia moja tu mwaka 2015.

Kwa mujibu wa UNIDO, uchimbaji wa mafuta huchangia karibu asilimia 90 ya sekta ya uchimabaji madini katika nchi zenye utajiri utokanao na mafuta. Bei ya mafuta ilishuka kutoka dola 109.5 mwaka 2012 hadi dola 49.5 mwaka 2015.

Aidha, ripoti hiyo inaonyesha kwamba kwa ujumla, uwezekano wa ukuaji unaotokana na bidhaa za madini unadidimia kwa sababu rasilmali za madini zenyewe zinapungua.