Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kila mtu angalikimbia kama wafanyavyo wasudani kusini- O’Brien

Kila mtu angalikimbia kama wafanyavyo wasudani kusini- O’Brien

Hali bado ni mbaya sana Sudan Kusini natoa wito kwa pande husika kusitisha mapigano na kuweka silaha zao chini.

Ni sehemu ya kauli ya Mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya usaidizi wa kibinadamu, OCHA Stephen O’Brien akizungumza na wanahabari hii leo mjini New York, Marekani baada ya ziara yake nchini humo.

Amesema wakati wa ziara hiyo alitembelea maeneo kadhaa ikiwemo Wau, na kushuhudia madhila ya wananchi sambamba na athari za mapigano ya hivi karibuni na kwamba.

(Sauti ya O’Brien)

“Watu Sudan Kusini siyo kwamba wanakimbia makazi yao kwa sababu tu eti wanataka chakula, huduma za afya au elimu kwa watoto wao! La hasha! Wanakimbia ili kuokoa maisha yao kama vile ambavyo wewe na mimi tungalikimbia iwapo tukikumbwa na vitisho vya kikatili.”

O’Brien amesema ni muhimu kuwalinda na kuwapatia msaada hasa kwenye maeneo ambako bado ni vigumu kufikia wahitaji.

image
Wakimbizi wa ndani huko Juba, Sudan Kusini,. (Picha:UN/Eric Kanalstein)
Kwa mantiki hiyo amesema wakati wa ziara alikutana na Rais Salva Kiir na viongozi wengine waandamizi wa serikali ya Sudan Kusini akiwemo Makamu wa Kwanza wa Rais nchini humo Taban Deng Gai ambaye kama wengine..

(Sauti ya O’Brien)

“Naye pia amehakikishia kuzingatia suala la kuwezesha kufikisha misaada ya kibinadamu, halikadhalika kuzingatia mchakato wa amani. Lakini kama nilivyosema kubadili maneno kuwa vitendo ni suala ambalo ni muhimu kufuatilia.”