Skip to main content

Uwekezaji vijijini wahitajika kukwamua walioathiriwa na Ebola- IFAD

Uwekezaji vijijini wahitajika kukwamua walioathiriwa na Ebola- IFAD

Rais wa Shirika la Kimataifa la Maendeleo ya Kilimo (IFAD), Kanayo Nwanze, amesema kuwa ingawa mlipuko mkubwa zaidi wa Ebola katika historia umeisha, uwekezaji unahitajika haraka vijijini nchini Sierra Leone na Liberia ili kuzisaidia nchi hizo kujikwamua tena.

Bwana Nwanze amesema hayo kabla ya ziara yake rasmi katika nchi hizo zilizoathiriwa na mlipuko wa Ebola, ambao uliwaua watu zaidi ya 11,300 Liberia, Guinea na Sierra Leone, kati ya 2014 na 2016.

Mkuu huyo wa IFAD amesema mlipuko wa Ebola ulikuwa na madhara makubwa kwa wakazi wa vijijini, wengi wao wakiwa wakulima wadogowadogo ambao hawakuweza kuzalisha chakula au kupata riziki wakati wa mlipuko huo.

Nwanze amesema iwapo uwekezaji hautaelekezwa vijijini sasa, wakulima hao huenda wakahama ili kutafuta ajira, na hivyo kuweka mashakani mustakhbali wa uhakika wa chakula.