Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkitaka kulinda sifa za nchi zenu, lindeni watoto- Ban

Mkitaka kulinda sifa za nchi zenu, lindeni watoto- Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, ametoa wito kwa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa na pande zinazoshiriki mizozo ziwalinde watoto, iwapo zinataka kulinda sifa zao.

Ban amesema hayo akilihutubia Baraza la Usalama, ambalo limefanya mjadala wa wazi kuhusu watoto na migogoro ya silaha.

Akizungumza kuhusu ripoti yake ya kila mwaka kuhusu watoto na migogoro ya silaha, Katibu Mkuu amesema yaliyomo katika ripoti hiyo hayatobadilishwa, kwani lengo ni kuwalinda watoto walioko hatarini kwa kuhakikisha kuna mabadiliko madhubuti.

“Picha ya usalama kimataifa inaendelea kubadilika, lakini kuna jambo moja pevu linalosalia dhahiri: watoto bado ndio wanaathirika zaidi wakati wa vita. Hata vita vina sheria. Shule na hospitali zinapaswa kulindwa. Raia wanapaswa kuepushwa. Watoto hawapaswi kutumikishwa katika mapigano.”

Ban ametoa wito kwa nchi zote wanachama ziyageuze maneno kuwa vitendo vinavyowalinda watoto kutokana na janga la migogoro ya vita sasa, na kuwaepusha wengine siku zijazo.