Katika siku ya kimataifa ya chui UM watoa wito kukabili uwindaji haramu

Katika siku ya kimataifa ya chui UM watoa wito kukabili uwindaji haramu

Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa mazingira UNEP kanda ya Asia na Pacific leo limeadhimisha siku ya kimataifa ya chui, kwa wito wa kuchukuliwa haraka hatua kuwalinda chui na kukabiliana na uwindaji haramu wa wanyama pori.

Kukiwa na asilimia ndogo tu ya wanyama hao waliosalia porini hususani barani Asia, Umoja wa mataifa umerejea wito wake wa kutovulilia hata kidogo uhalifu dhidi ya wanyama pori, wakati wa uzinduzi wa kampeni yake ya mwaka 2016 iitwayo “ Wild for Life”.

Kampeni hiyo ina lengo la kuchagiza mamilioni ya watu kote duniani kuchukua hatua binafsi kukomesha biashara haramu ya wanyama pori. Umoja huo umesema tishio kubwa kwa chui ni biashara ya nyama yao, ngozi yao na viungo vyao kwa ajili ya kutumika kwa dawa au tuzo.

Vitisho vingine ni kuendelea kutoweka kwa makazi yao kutokana na mvutano baiana ya wanyama hao na shughuli za binadamu, lakini vilevile mabadiliko ya tabia nchi.